Fermer le panneau de recherche

Appuyez sur Entrée pour rechercher ou ESC pour annuler.

Actes 21.8
Bible en Swahili de l’est


1 Ikawa tulipokwisha kujitenga nao na kuabiri, tukafika Kosi kwa tanga moja, na siku ya pili yake tukafika Rodo na kutoka huko tukafika Patara, 2 tukapata merikebu itakayovuka mpaka Foinike tukapanda tukatweka. 3 Na tulipoona Kipro tukaiacha upande wa kushoto; tukasafiri mpaka Shamu tukashuka Tiro. Kwa maana huko ndiko merikebu yetu itakakoshusha shehena yake. 4 Tukiisha kuwaona wanafunzi tukakaa huko siku saba, nao wakamwambia Paulo kwa uweza wa Roho asipande kwenda Yerusalemu. 5 Hata tulipotimiza siku zile tukaondoka tukaenda zetu, na watu wote, pamoja na wake zao na watoto wao, wakatusindikiza mpake nje ya mji, tukapiga magoti pwani tukaomba; 6 na baada ya kuagana tukapanda merikebuni, nao wakarudi kwao. 7 Hata tulipomaliza safari yetu kutoka Tiro tukafika Tolemai, tukawaamkua ndugu tukakaa kwao siku moja. 8 Asubuhi yake tukaondoka, tukafika Kaisaria, tukaingia nyumbani mwa Filipo, mhubiri wa Injili, aliyekuwa mmoja wa wale saba, tukakaa kwake. 9 Mtu huyu alikuwa na binti wanne, mabikira, waliokuwa wakitabiri. 10 Basi tulipokuwa tukikaa huko siku nyingi, nabii mmoja jina lake Agabo akashuka kutoka Uyahudi. 11 Alipotufikia akautwaa mshipi wa Paulo, akajifunga miguu na mikono, akasema, Roho Mtakatifu asema hivi, Hivyo ndivyo Wayahudi wa Yerusalemu watakavyomfunga mtu mwenye mshipi huu, nao watamtia katika mikono ya watu wa Mataifa. 12 Basi tuliposikia haya, sisi na watu wa mahali pale, tukamsihi asipande kwenda Yerusalemu. 13 Ndipo Paulo alipojibu, Mnafanya nini, kulia na kunivunja moyo? Kwa maana mimi, licha ya kufungwa, ni tayari hata kuuawa katika Yerusalemu kwa ajili ya jina lake Bwana Yesu. 14 Alipokataa shauri letu, tukanyamaza tukisema, Mapenzi ya Bwana na yatendeke. 15 Baada ya siku zile tukachukua vyombo vyetu tukapanda kwenda Yerusalemu. 16 Baadhi ya wanafunzi wa Kaisaria wakafuatana na sisi, wakamchukua na Mnasoni, mtu wa Kipro, mwanafunzi wa zamani ambaye ndiye tutakayekaa kwake. 17 Tulipofika Yerusalemu wale ndugu wakatukaribisha kwa furaha. 18 Hata siku ya pili yake Paulo akaingia kwa Yakobo pamoja nasi, na wazee wote walikuwako. 19 Na baada ya kuwaamkua, akawaeleza mambo yote moja moja Mungu aliyoyatenda katika Mataifa kwa huduma yake. 20 Nao waliposikia wakamtukuza Mungu, wakamwambia, Ndugu yetu, unaona jinsi Wayahudi walioamini walivyo elfu nyingi, nao wote wana wivu sana kwa ajili ya torati. 21 Nao wameambiwa habari zako, ya kwamba unawafundisha Wayahudi wote wakaao katika Mataifa kumwacha Musa, ukiwaambia wasiwatahiri watoto wao, wala wasizifuate desturi. 22 Basi, ni nini? Bila shaka watasikia kwamba umekuja. 23 Basi fanya neno hili tunalokuambia. Wako kwetu watu wanne waliofungwa na nadhiri. 24 Wachukue watu hao, ujitakase pamoja nao, na kuwagharimia ili wanyoe vichwa vyao, watu wote wapate kujua ya kuwa habari zile walizoambiwa juu yako si kitu, bali wewe mwenyewe unaenenda vizuri na kuishika torati. 25 Lakini kwa habari za watu wa Mataifa walioamini, tuliandika na kutoa hukumu yetu ya wao kujilinda nafsi zao na vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na damu, na kitu kilichosongolewa, na uasherati. 26 Ndipo Paulo akawatwaa wanaume wale, na siku ya pili yake akajitakasa nafsi yake pamoja nao, akaingia ndani ya hekalu, akitangaza habari ya kutimiza siku za utakaso, hata sadaka itolewe kwa ajili ya kila mmoja wao. 27 Basi zile siku saba zilipokuwa karibu kutimia, Wayahudi waliotoka Asia wakamwona ndani ya hekalu, wakawataharakisha watu wote, wakamkamata, 28 wakapiga kelele, na kusema, Enyi wanaume wa Israeli, tusaidieni. Huyu ndiye mtu yule afundishaye watu wote kila mahali kinyume cha taifa letu na torati na mahali hapa. Tena, zaidi ya haya, amewaingiza Wayunani katika hekalu, akapatia unajisi mahali hapa patakatifu. 29 Kwa maana walikuwa wamemwona Trofimo, Mwefeso, pamoja naye mjini, ambaye walidhania ya kuwa Paulo amemwingiza katika hekalu. 30 Mji wote ukataharuki, watu wakakutanika mbio mbio, wakamkamata Paulo, wakamkokota, wakamtoa hekaluni; mara milango ikafungwa. 31 Na walipokuwa wakitafuta njia ya kumwua, habari zikamfikilia jemadari wa kikosi ya kwamba Yerusalemu imechafuka, mji mzima. 32 Mara akatwaa askari na maakida, akawashukia mbio. Nao walipomwona jemadari na askari wakaacha kumpiga Paulo. 33 Kisha jemadari akakaribia, akamshika, akaamuru afungwe kwa minyororo miwili; akauliza, Nani huyu? Tena, amefanya nini? 34 Wengine katika makutano wakapiga kelele wakisema hivi, na wengine hivi. Basi alipokuwa hawezi kupata hakika ya habari kwa sababu ya zile kelele, akatoa amri aletwe ndani ya ngome. 35 Basi Paulo alipofika darajani ilikuwa kuchukuliwa na askari kwa sababu ya nguvu ya makutano. 36 Maana kundi kubwa la watu wakamfuata, wakipiga kelele, na kusema, Mwondoe huyu. 37 Naye alipokuwa analetwa ndani ya ngome, Paulo akamwambia jemadari, Nina ruhusa nikuambie neno? Naye akasema, Je! Unajua Kiyunani? 38 Wewe si yule Mmisri ambaye kabla ya siku hizi aliwafitinisha wale watu elfu nne, walioitwa Wauaji, akawaongoza jangwani? 39 Paulo akasema, Mimi ni mtu wa Kiyahudi, mtu wa Tarso, mji wa Kilikia, mwenyeji wa mji usiokuwa mnyonge. Nakuomba, nipe ruhusa niseme na wenyeji hawa. 40 Basi, alipompa ruhusa, Paulo akasimama madarajani, akawapungia mkono wale wenyeji; na ilipokuwa kimya kabisa, akanena nao kwa lugha ya Kiebrania, akisema,

Cette Bible est dans le domaine public.