Chapitre 15 Chapitre 17Annonce de l’exil et de la restauration
1 Tena neno la Bwana likanijia, kusema,
2 Wewe hutaoa mke, wala hutakuwa na wana wala binti mahali hapa.
3 Maana Bwana asema hivi, katika habari za wana, na katika habari za binti, wazaliwao mahali hapa, na katika habari za mama zao waliowazaa, na katika habari za baba zao waliowazaa, katika nchi hii;
4 watakufa kwa maradhi mabaya; hawataliliwa, wala hawatazikwa; watakuwa kama samadi juu ya uso wa nchi; nao wataangamizwa kwa upanga, na kwa njaa; na mizoga yao itakuwa chakula cha ndege wa angani, na cha wanyama wa nchi.
5 Maana Bwana asema hivi, Usiingie ndani ya nyumba yenye matanga, wala usiende kuwaombolezea, wala kuwalilia; maana nimewaondolea watu hawa amani yangu, asema Bwana, hata fadhili zangu na rehema zangu.
6 Wakubwa kwa wadogo wote pia watakufa katika nchi hii; hawatazikwa, wala watu hawatawalilia, wala kujikata-kata kwa ajili yao, wala kujinyoa kwa ajili yao;
7 wala watu hawatamega mkate kwa ajili yao, wakati wa kuomboleza, ili kuwafariji kwa ajili yao waliokufa; wala watu hawatawapa kikombe cha faraja, wanywe kwa ajili ya baba yao au mama yao.
8 Wala usiingie ndani katika nyumba yenye karamu, kuketi pamoja nao, na kula na kunywa.
9 Maana Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Mimi, mbele ya macho yenu, na katika siku zenu, nitaikomesha sauti ya furaha, na sauti ya kicheko, mahali hapa; sauti ya bwana arusi, na sauti ya bibi arusi.
10 Tena itakuwa, utakapowaonyesha watu hawa maneno haya yote, nao wakakuambia, Mbona Bwana amenena juu yetu mabaya haya makuu? Uovu wetu ni uovu gani? Na dhambi yetu, tuliyomtenda Bwana, Mungu wetu, ni nini?
11 Ndipo utakapowaambia, Ni kwa sababu baba zenu wameniacha mimi, asema Bwana, na kuwafuata miungu mingine, na kuwatumikia, na kuwaabudu, wakaniacha mimi, wasiishike torati yangu;
12 na ninyi mmetenda mabaya kupita baba zenu; maana angalieni, mnaenenda kila mmoja wenu kwa ushupavu wa moyo wake mbaya, msinisikilize mimi;
13 basi, kwa sababu hiyo, nitawatoeni katika nchi hii, na kuwaingiza katika nchi ambayo hamkuijua, wala ninyi wala baba zenu; na huko mtawatumikia miungu mingine mchana na usiku; kwa maana mimi sitawapa fadhili zangu hata kidogo.
14 Kwa hiyo, angalia, siku zinakuja, asema Bwana, ambapo hawatasema tena, Aishivyo Bwana, aliyewaleta wana wa Israeli toka nchi ya Misri;
15 lakini, Aishivyo Bwana, aliyewaleta wana wa Israeli toka nchi ya kaskazini, na toka nchi zote alikowafukuza; nami nitawarudisha katika nchi yao wenyewe niliyowapa baba zao. 16 Tazama, asema Bwana, Nitatuma watu kuwaita wavuvi wengi, nao watawavua; na baada ya hayo nitatuma watu kuwaita wawindaji wengi, nao watawawinda, watoke katika kila mlima, na kila kilima, na pango za majabali.
17 Maana macho yangu yaziangalia njia zao zote, hawakufichwa uso wangu usiwaone, wala haukusitirika uovu wao macho yangu yasiuone.
18 Nami kwanza nitawalipa uovu wao na dhambi zao maradufu, kwa kuwa wameitia unajisi nchi yangu, kwa mizoga ya vitu vyao vichukizavyo, na kuujaza urithi wangu kwa machukizo yao.
19 Ee Bwana, nguvu zangu, ngome yangu, na kimbilio langu siku ya taabu, kwako wewe watakuja mataifa yote toka ncha za dunia, wakisema, Baba zenu hawakurithi kitu ila uongo, naam, ubatili na vitu visivyofaa.
20 Je! Mwanadamu ajifanyie miungu, wasio miungu?
21 Basi, tazama, nitawajulisha, mara moja hii nitawajulisha, mkono wangu, na nguvu zangu; nao watajua ya kuwa, jina langu ni YEHOVA.