Un clic sur un verset envoie vers le comparateur de versions.
Luc 20.33 Bible en Swahili de l’est
1 Ikawa siku moja, alipokuwa akiwafundisha watu hekaluni, na kuihubiri habari njema, wakuu wa makuhani na waandishi pamoja na wazee walimtokea ghafula; 2 wakamwambia, wakisema, Tuambie, unatenda mambo hayo kwa mamlaka gani? Tena, ni nani aliyekupa mamlaka hii? 3 Akajibu akawaambia, Nami nitawauliza ninyi neno moja; niambieni, 4 Ubatizo wa Yohana, je! Ulitoka mbinguni au kwa wanadamu? 5 Wakahojiana wao kwa wao, wakisema, Kama tukisema ulitoka mbinguni, atasema, Basi, mbona hamkumwamini? 6 Na tukisema ulitoka kwa wanadamu, watu wote watatupiga kwa mawe, kwa kuwa wamemkubali Yohana kuwa ni nabii. 7 Wakajibu, kwamba, Hatujui ulikotoka. 8 Yesu akawaambia, Wala mimi siwaambii ninyi ni kwa mamlaka gani ninatenda mambo haya. 9 Akaanza kuwaambia watu mfano huu; Mtu mmoja alipanda shamba la mizabibu; akapangisha wakulima, akaenda akakaa katika nchi nyingine muda mrefu. 10 Na wakati wa mavuno alituma mtumwa kwa wale wakulima ili wampe baadhi ya matunda ya mizabibu; wakulima wakampiga wakamfukuza mikono mitupu. 11 Akatuma na mtumwa mwingine. Wakampiga huyu naye, wakamwaibisha wakamfukuza mikono mitupu. 12 Akamtuma na wa tatu; huyu naye wakamtia jeraha, wakamtupa nje. 13 Basi, bwana wa shamba la mizabibu alisema, Nifanyeje? Nitamtuma mwanangu, mpendwa wangu; yamkini watamheshimu yeye. 14 Lakini, wale wakulima walipomwona, walishauriana wao kwa wao, wakisema, Huyu ndiye mrithi; haya, na tumwue, ili urithi uwe wetu. 15 Wakamtupa nje ya shamba la mizabibu, wakamwua. Basi, bwana wa shamba la mizabibu atawatendeje? 16 Atakuja na kuwaangamiza wakulima wale, na lile shamba la mizabibu atawapa wengine. Waliposikia hayo walisema, Hasha! Yasitukie haya! 17 Akawakazia macho akasema, Maana yake nini basi neno hili lililoandikwa, Jiwe walilolikataa waashi, Hilo limekuwa jiwe kuu la pembeni? 18 Kila mtu aangukaye juu ya jiwe hilo atavunjika-vunjika; na ye yote ambaye litamwangukia litamsaga kabisa. 19 Nao waandishi na wakuu wa makuhani walitafuta kumkamata saa iyo hiyo, wakawaogopa watu, maana walitambua ya kwamba mfano huu amewanenea wao. 20 Wakamvizia-vizia, wakatuma wapelelezi waliojifanya kuwa watu wa haki, ili wamnase katika maneno yake, wapate kumtia katika enzi na mamlaka ya liwali. 21 Wakamwuliza, wakisema, Mwalimu, twajua ya kwamba wasema na kufundisha yaliyo ya haki, wala hujali cheo cha mtu, bali unafundisha njia ya Mungu kwa kweli. 22 Je! Ni halali tumpe Kaisari kodi, au sivyo? 23 Lakini yeye alitambua hila yao, akawaambia, 24 Nionyesheni dinari. Ina sura na anwani ya nani? Wakamjibu, Ya Kaisari. 25 Akawaambia, Basi, vya Kaisari mpeni Kaisari, na vya Mungu mpeni Mungu. 26 Wala hawakuweza kumshitaki kwa maneno yake mbele ya watu; wakastaajabia majibu yake, wakanyamaa. 27 Kisha baadhi ya Masadukayo wakamwendea, wale wasemao ya kwamba hakuna ufufuo, wakamwuliza, 28 wakisema, Mwalimu, Musa alituandikia ya kuwa, mtu akifiwa na ndugu yake mwenye mke, lakini hana mtoto na amtwae huyu mke, ampatie ndugu yake mzao. 29 Basi, kulikuwa na ndugu saba. Wa kwanza alioa mke, akafa hana mtoto; 30 na wa pili [akamtwaa yule mke, akafa hana mtoto;] 31 hata wa tatu akamwoa, na kadhalika wote saba, wakafa, wasiache watoto. 32 Mwisho akafa yule mke naye.33 Basi, katika ufufuo atakuwa mke wa yupi? Maana aliolewa na wote saba.34 Yesu akawaambia, Wana wa ulimwengu huu huoa na kuolewa; 35 lakini, wale wahesabiwao kuwa wamestahili kuupata ulimwengu ule, na kule kufufuka katika wafu, hawaoi wala hawaolewi; 36 wala hawawezi kufa tena; kwa sababu huwa sawasawa na malaika, nao ni wana wa Mungu, kwa vile walivyo wana wa ufufuo. 37 Lakini, ya kuwa wafu hufufuliwa, hata na Musa alionyesha katika sura ya Kijiti, hapo alipomtaja Bwana kuwa ni Mungu wa Ibrahimu, na Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo. 38 Naye si Mungu wa wafu, bali wa walio hai; kwa kuwa wote huishi kwake. 39 Waandishi wengine wakajibu wakamwambia, Mwalimu, umesema vema; 40 wala hawakuthubutu kumwuliza neno baada ya hayo. 41 Akawaambia, Wasemaje watu kwamba Kristo ni Mwana wa Daudi? 42 Maana, Daudi mwenyewe asema katika chuo cha Zaburi, Bwana alimwambia Bwana wangu, Uketi mkono wangu wa kuume, 43 Hata niwaweke adui zako Kuwa kiti cha kuwekea miguu yako. 44 Basi Daudi amwita Bwana; amekuwaje mwana wake? 45 Na watu wote walipokuwa wakimsikiliza, aliwaambia wanafunzi wake, 46 Jilindeni na waandishi, wapendao kutembea wamevaa mavazi marefu, na kusalimiwa masokoni, na kuketi mbele katika masinagogi, na viti vya mbele karamuni. 47 Wanakula nyumba za wajane, na kwa unafiki husali sala ndefu. Hao watapata hukumu iliyo kuu.