Chapitre 25 Chapitre 27Isaac à Guérar
1 Ikawa njaa katika nchi hiyo, mbali na njaa ile ya kwanza iliyokuwa siku za Ibrahimu. Isaka akamwendea Abimeleki, mfalme wa Wafilisti, huko Gerari.
2 Bwana akamtokea, akasema, Usishuke kwenda Misri, kaa katika nchi nitakayokuambia.
3 Kaa ugenini katika nchi hiyo, nami nitakuwa pamoja nawe, na kukubariki, maana nitakupa wewe na uzao wako nchi hizi zote. Nami nitakifanya imara kiapo nilichomwapia Ibrahimu baba yako.
4 Nitazidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, nami nitawapa uzao wako nchi hizi zote, na katika uzao wako mataifa yote ya dunia watajibarikia.
5 Kwa sababu Ibrahimu alisikia sauti yangu, akayahifadhi maagizo yangu, na amri zangu, na hukumu zangu, na sheria zangu.
6 Isaka akakaa katika Gerari.
7 Watu wa mahali hapo wakamwuliza habari za mkewe. Akasema, Ni ndugu yangu huyu maana aliogopa kusema, Ni mke wangu, watu wa nchi wasije wakamwua kwa ajili ya Rebeka; kwa maana alikuwa mzuri wa uso.
8 Ikawa alipokuwa amekaa huko siku nyingi, Abimeleki, mfalme wa Wafilisti, akachungulia dirishani, akamwona Isaka anacheza-cheza na Rebeka mkewe.
9 Abimeleki akamwita Isaka, akasema, Yakini huyu ni mkeo, mbona ulisema, Ni ndugu yangu huyu? Isaka akamwambia, Kwa sababu nalisema, Nisife kwa ajili yake.
10 Abimeleki akasema, Ni nini hii uliyotutendea? Labda mtu mmojawapo angalilala na mkeo bila kufikiri, nawe ungalitutia hatiani. 11 Basi Abimeleki akawaamuru watu wote, akisema, Amgusaye mtu huyu au mkewe lazima atauawa.
12 Isaka akapanda mbegu katika nchi ile, akapata mwaka ule vipimo mia kwa kimoja, Bwana akambariki.
13 Na mtu huyu akawa mkuu, akazidi kusitawi, hata akawa mkuu sana.
14 Akawa na mali ya kondoo, na mali ya ng’ombe, na watumwa wengi. Hao Wafilisti wakamhusudu.
15 Na vile visima vyote walivyochimba watumwa wa baba yake, siku za Ibrahimu babaye, Wafilisti walikuwa wamevifukia, wakavijaza kifusi.
16 Abimeleki akamwambia Isaka, Utoke kwetu, maana wewe una nguvu sana kuliko sisi.
17 Basi Isaka akatoka huko akapiga kambi katika bonde la Gerari, akakaa huko.
18 Isaka akarudi akavichimbua vile visima vya maji walivyovichimba siku za Ibrahimu babaye; maana wale Wafilisti walikuwa wamevifukia baada ya kufa kwake Ibrahimu; naye akaviita majina kufuata majina alivyoviita babaye.
19 Watumwa wa Isaka wakachimba katika lile bonde, wakapata kisima cha maji yanayobubujika.
20 Wachungaji wa Gerari wakagombana na wachungaji wa Isaka wakisema, Maji haya ni yetu. Ndipo akakiita jina la kile kisima Eseki, kwa sababu waligombana naye.
21 Wakachimba kisima kingine, wakagombania na hicho tena. Akakiita jina lake Sitna.
22 Akaondoka huko akachimba kisima kingine, wala hicho hawakukigombania. Akakiita jina lake Rehobothi, akasema, Kwa kuwa sasa Bwana ametufanyia nafasi, nasi tutazidi katika nchi.
23 Akapanda kutoka hapo mpaka Beer-sheba.
24 Bwana akamtokea usiku uleule, akasema, Mimi ni Mungu wa Ibrahimu baba yako, usiogope, maana mimi ni pamoja nawe, nami nitakubarikia, na kuzidisha uzao wako kwa ajili ya Ibrahimu mtumishi wangu.
25 Akajenga madhabahu huko, akaliitia jina la Bwana. Akapiga hema yake huko, na watumwa wa Isaka wakachimba kisima huko.
26 Ndipo Abimeleki akamwendea kutoka Gerari, pamoja na Ahuzathi rafiki yake, na Fikoli, jemadari wa jeshi lake.
27 Isaka akawauliza, Mbona mwanijia, nanyi mmenichukia, mkanifukuza kwenu?
28 Wakasema, Hakika tuliona ya kwamba Bwana alikuwa pamoja nawe; nasi tukasema, Na tuapiane, sisi na wewe, na kufanya mapatano nawe
29 ya kuwa hutatutenda mabaya, iwapo sisi hatukukugusa wewe, wala hatukukutendea ila mema, tukakuacha uende zako kwa amani; nawe sasa u mbarikiwa wa Bwana.
30 Basi akawafanyia karamu, nao wakala, wakanywa.
31 Wakaondoka asubuhi na mapema, wakaapiana wao kwa wao, kisha Isaka akawapa ruhusa, nao wakaenda zao kwa amani.
32 Ikawa siku ileile, watumwa wa Isaka wakaja wakampasha habari za kile kisima walichokuwa wamekichimba, wakamwambia, Tumeona maji.
33 Naye akakiita jina lake Shiba; kwa hiyo jina la mji huo ni Beer-sheba, hata leo.
34 Esau alipokuwa mwenye miaka arobaini, akamwoa Yudithi, binti Beeri, Mhiti, na Basemathi, binti Eloni, Mhiti.
35 Roho zao Isaka na Rebeka zikajaa uchungu kwa ajili yao.