Un clic sur un verset envoie vers le comparateur de versions.
Jérémie 35.10 Bible en Swahili de l’est
1 Neno hili ndilo lililomjia Yeremia, kutoka kwa Bwana, katika siku za Yehoyakimu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda, kusema, 2 Enenda nyumbani kwa Warekabi, ukanene nao, ukawalete nyumbani kwa Bwana, katika chumba kimoja, ukawape divai wanywe. 3 Basi nikamtwaa Yaazania, mwana wa Yeremia, mwana wa Habasinia, na ndugu zake, na wanawe wote, na nyumba yote ya Warekabi; 4 nikawaleta ndani ya nyumba ya Bwana, ndani ya chumba cha wana wa Hanani, mwana wa Igdalia, mtu wa Mungu, kilichokuwa karibu na chumba cha wakuu, nacho kilikuwa juu ya chumba cha Maaseya, mwana wa Shalumu, bawabu; 5 nikaweka mabakuli yaliyojaa divai, na vikombe, mbele ya wana wa nyumba ya Warekabi, nikawaambia, Nyweni divai. 6 Lakini wakasema, Hatutakunywa divai; kwa maana Yonadabu, mwana wa Rekabu, baba yetu, alituamuru, akisema, Msinywe divai, ninyi wala wana wenu, hata milele; 7 wala msijenge nyumba, wala msipande mbegu, wala msipande mizabibu, wala msiwe nayo; bali siku zenu zote mtakaa katika hema; mpate kuishi siku nyingi katika nchi ambayo mtakaa ndani yake hali ya wageni. 8 Nasi tumeitii sauti ya Yonadabu, mwana wa Rekabu, baba yetu, katika yote aliyotuamuru, kwamba tusinywe divai siku zetu zote, sisi, na wake zetu, na wana wetu, na binti zetu; 9 wala tusijijengee nyumba za kukaa; wala hatuna shamba la mizabibu, wala konde, wala mbegu;10 bali tumekaa katika hema, nasi tumetii; tukafanya sawasawa na yote aliyotuamuru Yonadabu, baba yetu.11 Lakini ikawa, Nebukadreza, mfalme wa Babeli, alipopanda akaingia nchi hii, ndipo tukasema, Haya! Twende Yerusalemu, tukiliogopa jeshi la Wakaldayo, na tukiliogopa jeshi la Washami; basi hivyo tunakaa Yerusalemu. 12 Ndipo neno la Bwana likamjia Yeremia, kusema, 13 Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Enenda ukawaambie wana wa Yuda, na wenyeji wa Yerusalemu, Je! Hamtaki kupokea mafundisho, myasikilize maneno yangu? Asema Bwana. 14 Maneno ya Yonadabu, mwana wa Rekabu, aliyowaamuru wanawe, kwamba wasinywe divai, yametimizwa, na hata leo hawanywi; maana waitii hiyo amri ya baba yao; lakini mimi nimesema nanyi, nikiamka mapema na kunena, bali ninyi hamkunisikiliza mimi. 15 Pia naliwapeleka watumishi wangu wote, manabii, kwenu ninyi, nikiamka mapema na kuwapeleka, nikisema, Rudini sasa, kila mtu na aiache njia yake mbaya, mkatengeneze matendo yenu, wala msiwafuate miungu mingine, ili kuwatumikia, nanyi mtakaa katika nchi hii, niliyowapa ninyi na baba zenu; lakini hamkutega masikio yenu, wala hamkunisikiliza. 16 Basi, kwa kuwa wana wa Yonadabu, mwana wa Rekabu, wameitimiza amri ya baba yao aliyowaamuru, lakini watu hawa hawakunisikiliza mimi; 17 kwa sababu hiyo, asema Bwana, Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli; Tazama nitaleta juu ya Yuda, na juu ya wenyeji wote wa Yerusalemu, mabaya yote niliyoyatamka juu yao; kwa sababu nimesema nao, wasinisikilize; nimewaita, wala hawakuniitikia. 18 Naye Yeremia akawaambia watu wa nyumba ya Warekabi, Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Kwa sababu mmeitii amri ya Yonadabu, baba yenu, na kuyashika maagizo yake yote, na kutenda sawasawa na yote aliyowaamuru; 19 basi, kwa sababu hiyo, Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Yonadabu, mwana wa Rekabu, hatakosa kuwa na mtu wa kusimama mbele zangu hata milele.