Fermer le panneau de recherche

Appuyez sur Entrée pour rechercher ou ESC pour annuler.

Proverbes 21.9
Bible en Swahili de l’est


1 Moyo wa mfalme huwa katika mkono wa Bwana; Kama mifereji ya maji huugeuza po pote apendapo. 2 Kila njia ya mtu ni sawa machoni pake mwenyewe; Bali Bwana huipima mioyo. 3 Kutenda haki na hukumu Humpendeza Bwana kuliko kutoa sadaka. 4 Macho yenye kiburi, na moyo wa kutakabari, Hata ukulima wa waovu, ni dhambi. 5 Mawazo ya wenye bidii huuelekea utajiri tu; Bali kila mwenye pupa huuelekea uhitaji. 6 Kupata akiba ya mali kwa ulimi wa uongo Ni moshi upeperushwao; ni kutafuta mauti. 7 Jeuri ya wabaya itawaondolea mbali; Kwa sababu wamekataa kutenda hukumu. 8 Njia yake aliyelemewa na dhambi imepotoka sana; Bali mtu aliye safi, kazi yake ni sawasawa. 9 Ni afadhali kukaa katika pembe ya darini, Kuliko katika nyumba pana pamoja na mwanamke mgomvi. 10 Nafsi ya mtu mbaya hutamani uovu; Jirani yake hapati fadhili machoni pake. 11 Mwenye mzaha aadhibiwapo, mjinga hupata hekima; Na mwenye hekima afundishwapo, hupokea maarifa. 12 Mwenye haki huitafakari nyumba ya mtu mbaya; Jinsi wabaya waangushwavyo wakaangamia. 13 Azibaye masikio yake asisikie kilio cha maskini, Yeye naye atalia, lakini hatasikiwa. 14 Kipawa cha siri hutuliza hasira; Na rushwa bindoni humliza ghadhabu kali. 15 Ni furaha yao wenye haki kutenda hukumu; Lakini ni uharibifu kwao watendao maovu. 16 Mtu aikosaye njia ya busara Atakaa katika mkutano wao waliokufa. 17 Mtu apendaye anasa atakuwa maskini; Apendaye mvinyo na mafuta hatakuwa tajiri. 18 Mtu asiye haki ni fidia ya wenye haki; Naye afanyaye hila ni badala ya watu wa adili. 19 Ni afadhali kukaa katika nchi ya nyika; Kuliko na mwanamke mgomvi, mchokozi. 20 Kuna hazina ya thamani na mafuta katika maskani ya mwenye hekima; Bali mwanadamu aliye mpumbavu huyameza. 21 Aandamaye haki na fadhili, Ataona uhai na haki na heshima. 22 Mwenye hekima huupandia mji wao wenye nguvu; Na kuziangusha nguvu za tumaini lao. 23 Mtu azuiaye kinywa chake na ulimi wake, Atajilinda nafsi yake na taabu. 24 Mwenye kiburi na kutakabari, jina lake ni mbishi; Hutenda mambo katika majivuno ya kiburi chake. 25 Matakwa yake mtu mvivu humfisha, Kwa maana mikono yake hukataa kufanya kazi. 26 Kuna atamaniye kwa choyo mchana kutwa; Bali mwenye haki hutoa wala hanyimi. 27 Sadaka ya wasio haki ni chukizo; Si zaidi sana ailetapo mwenye nia mbaya! 28 Shahidi wa uongo atapotea; Bali mtu asikiaye atasema maneno yadumuyo. 29 Asiye haki huufanya uso wake kuwa mgumu; Bali mtu mnyofu huzifikiri njia zake. 30 Hapana hekima, wala ufahamu, Wala shauri, juu ya Bwana. 31 Farasi huwekwa tayari kwa siku ya vita; Lakini Bwana ndiye aletaye wokovu.

Cette Bible est dans le domaine public.