Un clic sur un verset envoie vers le comparateur de versions.
Esaïe 33 Bible en Swahili de l’est
1 Ole wako uharibuye ila hukuharibiwa, utendaye hila wala hukutendwa hila! Utakapokwisha kuharibu, utaharibiwa wewe; na utakapokwisha kutenda kwa hila, wao watakutenda hila wewe. 2 Ee Bwana, uturehemu; tumekungoja wewe; uwe wewe mkono wetu kila asubuhi,na wokovu wetu pia wakati wa taabu. 3 Kabila za watu wamekimbia wakisikia kelele za fujo; mataifa wametawanyika ulipojiinua nafsi yako. 4 Na mateka yako yatakumbwa kama wadudu wakumbavyo, wataruka juu yake kama arukavyo nzige. 5 Bwana ametukuka; kwa maana anakaa juu; amejaza Sayuni hukumu na haki. 6 Nyakati zako zitakuwa nyakati za kukaa imara; za wokovu tele na hekima na maarifa; kumcha Bwana ni hazina yake ya akiba. 7 Angalia, mashujaa wao wanalia nje, wajumbe wa amani wanalia kwa uchungu. 8 Njia kuu zimeachwa, msafiri amekoma; ameyavunja maagano, ameidharau miji, hamjali mtu. 9 Nchi inaomboleza, na kulegea; Lebanoni imetahayarika na kunyauka; Sharoni imekuwa kama jangwa; Bashani na Karmeli zimepukutika majani. 10 Basi, sasa nitasimama; asema Bwana; sasa nitajiinua, sasa nitajitukuza. 11 Ninyi mtachukua mimba ya makapi, mtazaa majani makavu; pumzi yenu ni moto utakaowateketeza wenyewe. 12 Nao mataifa watakuwa kama kuchoma chokaa, kama miiba iliyokatika, iteketezwayo motoni. 13 Sikieni, ninyi mlio mbali, niliyoyatenda; na ninyi mlio karibu, kirini uweza wangu. 14 Wenye dhambi walio katika Sayuni wanaogopa; tetemeko limewashika wasiomcha Mungu; Ni nani kwetu sisi awezaye kukaa na moto ulao; ni nani kwetu sisi awezaye kukaa na moto uteketezao milele? 15 Ni yeye aendaye kwa haki, anenaye maneno ya adili; ni yeye anayedharau faida ipatikanayo kwa dhuluma; akung’utaye mikono yake asipokee rushwa; azibaye masikio yake asisikie habari za damu; afumbaye macho yake asitazame uovu. 16 Huyu ndiye atakayekaa juu; majabali ni ngome yake; atapewa chakula chake; maji yake hayatakoma. 17 Macho yako yatamwona mfalme katika uzuri wake, yataona nchi iliyoenea sana. 18 Moyo wako utatafakari hofu ile; Yuko wapi yeye aliyehesabu? Yuko wapi yeye aliyeupima ushuru? Yuko wapi yeye aliyeihesabu minara? 19 Hutawaona watu wale wakali; watu wa maneno magumu usiyoweza kuyafahamu; wenye lugha ya kigeni usiyoweza kuelewa nayo. 20 Angalia Sayuni, mji wa sikukuu zetu; macho yako yatauona Yerusalemu umekuwa kao la raha; hema isiyotanga-tanga; vigingi vyake havitang’olewa, wala kamba zake hazitakatika. 21 Bali huko Bwana atakuwa pamoja nasi, mwenye adhama; mahali penye mito mipana na vijito, pasipopita mashua na makasia yake; wala hapana merikebu ya vita itakayopita hapo. 22 Kwa maana Bwana ndiye mwamuzi wetu; Bwana ndiye mfanya sheria wetu; Bwana ndiye mfalme wetu; ndiye atakayetuokoa. 23 Kamba zako zimelegea; hawakuweza kukaza sana shina la mlingoti wao; hawakuweza kulikunjua tanga; ndipo mapato ya mateka yaligawanywa, hata wachechemeao walipata mateka. 24 Wala hapana mwenyeji atakayesema, Mimi mgonjwa; watu wakaao humo watasamehewa uovu wao.