Fermer le panneau de recherche

Appuyez sur Entrée pour rechercher ou ESC pour annuler.

Esaïe 56
Bible en Swahili de l’est


1 Bwana asema hivi, Shikeni hukumu, mkatende haki; kwa maana wokovu wangu u karibu kuja, na haki yangu kufunuliwa. 2 Heri afanyaye haya, na mwanadamu ayashikaye sana; azishikaye sabato asizivunje, auzuiaye mkono wake usifanye uovu wo wote. 3 Wala mgeni, aambatanaye na Bwana, asiseme hivi, Hakika yake Bwana atanitenga na watu wake; wala towashi asiseme, Mimi ni mti mkavu. 4 Kwa maana Bwana awaambia hivi matowashi, wanaozishika sabato zangu, na kuyachagua mambo yanipendezayo, na kulishika sana agano langu; 5 Nitawapa hawa nyumbani mwangu, na ndani ya kuta zangu, kumbukumbu na jina, lililo jema kuliko kuwa na wana na binti; nitawapa jina lidumulo milele, lisilokatiliwa mbali. 6 Na wageni, walioandamana na Bwana ili wamhudumu, na kulipenda jina la Bwana, kuwa watumishi wake; kila aishikaye sabato asiivunje, na kulishika sana agano langu; 7 Nitawaleta hao nao hata mlima wangu mtakatifu, na kuwafurahisha katika nyumba yangu ya sala; makafara yao na dhabihu zao zitakubaliwa juu ya madhabahu zangu; kwa maana nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa yote. 8 Bwana MUNGU, akusanyaye waliofukuzwa katika Israeli asema, Pamoja na hayo nitamkusanyia na wengine, zaidi ya hao walio wake waliokusanywa. 9 Enyi hayawani wote wa nyikani, njoni, Mle, enyi hayawani wote wa mwituni. 10 Walinzi wake ni vipofu, wote pia hawana maarifa; wote ni mbwa walio bubu, hawawezi kulia; huota ndoto, hulala, hupenda usingizi. 11 Naam, mbwa hao wana choyo sana, hawashibi kamwe; na hao ni wachungaji wasioweza kufahamu neno; wote pia wamegeuka upande, wazifuate njia zao wenyewe, kila mmoja kwa faida yake, toka pande zote. 12 Husema, Njoni, nitaleta divai, Na tunywe sana kileo; Na kesho itakuwa kama leo, Sikukuu kupita kiasi.

Cette Bible est dans le domaine public.