Fermer le panneau de recherche

Appuyez sur Entrée pour rechercher ou ESC pour annuler.

Esaïe 46.1
Bible en Swahili de l’est


1 Beli anaanguka chini, Nebo anainama; sanamu zao ziko juu ya wanyama, na juu ya ng’ombe; vitu vile mlivyokuwa mkivichukua huku na huku vimekuwa mzigo, mzigo wa kumlemea mnyama aliyechoka. 2 Wanajiinamisha, wanainama pamoja; hawakuweza kuutua mzigo, bali wao wenyewe wamekwenda kufungwa. 3 Nisikilizeni, enyi wa nyumba ya Yakobo, ninyi mlio mabaki ya nyumba ya Israeli, mliochukuliwa nami tangu tumboni, mlioinuliwa tangu mimbani; 4 na hata uzee wenu mimi ndiye, na hata wakati wenu wa mvi nitawachukueni; nimefanya, nami nitachukua; naam, nitachukua na kuokoa. 5 Mtanifananisha na nani, na kunisawazisha naye, na kunilinganisha naye, ili tuwe sawasawa? 6 Watu wamwagao dhahabu kutoka mfukoni, na kupima fedha katika mizani, huajiri mfua dhahabu, akaifanya mungu; huanguka, naam, huabudu. 7 Humchukua begani, humchukua, wakamsimamisha mahali pake, akasimama; hataondoka katika mahali pake, naam, mmoja atamwita, lakini hawezi kujibu, wala kumwokoa na taabu yake. 8 Kumbukeni haya, mkajionyeshe kuwa waume; jifahamisheni haya, ninyi mkosao; 9 kumbukeni mambo ya zamani za kale; maana mimi ni Mungu, wala hapana mwingine; mimi ni Mungu, wala hapana aliye kama mimi; 10 nitangazaye mwisho tangu mwanzo, na tangu zamani za kale mambo yasiyotendeka bado; nikisema, Shauri langu litasimama, nami nitatenda mapenzi yangu yote. 11 Nikiita ndege mkali kutoka mashariki, mtu wa shauri langu toka nchi iliyo mbali; naam, nimenena, nami nitatekeleza; nimekusudia, nami nitafanya. 12 Nisikilizeni, ninyi mlio na moyo mshupavu, mlio mbali na haki; 13 Mimi ninaleta karibu haki yangu, haitakuwa mbali, na wokovu wangu hautakawia; nami nitaweka wokovu katika Sayuni kwa ajili ya Israeli, utukufu wangu.

Cette Bible est dans le domaine public.