Fermer le panneau de recherche

Appuyez sur Entrée pour rechercher ou ESC pour annuler.

Psaumes 90.15
Bible en Swahili de l’est


Quatrième livre

La brièveté de la vie humaine

1 Wewe, Bwana, umekuwa makao yetu, Kizazi baada ya kizazi.
2 Kabla haijazaliwa milima, wala hujaiumba dunia, Na tangu milele hata milele ndiwe Mungu.
3 Wamrudisha mtu mavumbini, usemapo, Rudini, enyi wanadamu.
4 Maana miaka elfu machoni pako Ni kama siku ya jana ikiisha kupita, Na kama kesha la usiku.
5 Wawagharikisha, huwa kama usingizi, Asubuhi huwa kama majani yameayo.
6 Asubuhi yachipuka na kumea, Jioni yakatika na kukauka.
7 Maana tumetoweshwa kwa hasira yako, Na kwa ghadhabu yako tumefadhaishwa.
8 Umeyaweka maovu yetu mbele zako, Siri zetu katika mwanga wa uso wako.
9 Maana siku zetu zote zimepita katika hasira yako, Tumetowesha miaka yetu kama kite.
10 Siku za miaka yetu ni miaka sabini, Na ikiwa tuna nguvu miaka themanini; Na kiburi chake ni taabu na ubatili, Maana chapita upesi tukatokomea mara.
11 Ni nani aujuaye uweza wa hasira yako? Na ghadhabu yako kama ipasavyo kicho chako?
12 Basi, utujulishe kuzihesabu siku zetu, Tujipatie moyo wa hekima.
13 Ee Bwana urudi, hata lini? Uwahurumie watumishi wako.
14 Utushibishe asubuhi kwa fadhili zako, Nasi tutashangilia na kufurahi siku zetu zote.
15 Utufurahishe kwa kadiri ya siku ulizotutesa, Kama miaka ile tuliyoona mabaya.
16 Matendo yako na yaonekane kwa watumishi wako, Na adhama yako kwa watoto wao.
17 Na uzuri wa Bwana, Mungu wetu, uwe juu yetu, Na kazi ya mikono yetu utufanyie thabiti, Naam, kazi ya mikono yetu uithibitishe.

Cette Bible est dans le domaine public.